Na Ally Mbarouk
Pemba Peremba!
Pemba Peremba!
Pengine kwa wakaazi wa Zanzibar mengi tumeshayasikia kuhusa mji unaoitwa Miembeni .Hapa zizungumzii miembeni ya Pemba banda taka , aaah , wala sizungumzii Miembeni ya Mkoani , ni Miembeni ya
Unguja ;mkabala na
Michenzani ...nyote mnapajua . Basi kama umeshasikia na umeshapajua hebu panda boti . Sikupandishi Serengeti ukalala baharini nakupandisha ndege mpya ya Air Zahra au sijui Zara..ufike mara moja . Ukifika uwanja wa ndege chukua tax hadi Machomane .Ama kama miji ingalipewa majina kulingana na tabia za mitaa hii ningaliita Miembeni ya Pemba .
Nisikuzungushe : mara amba Serengeti , mara Air Zara mara Machomane , hebu tuende katika wazo nililolifikiria katika makala haya . Pengine nimenasibisha mitaa ya Miembeni na Machomane Pemba kwa vitabia na vijitabia fulani fulani hivi vya mitaa . Si unayakumbuka mambo yetu yalee tuliyozoea;yanayowafanya vijana kutoka mate, kuwa machizi taahira .Mambo yale yanayowafanya vijana kukosa dira ya maisha na na kuwa mazoba , ombaomba na vibaka wakubwa mitaani .Mambo ya enzi zile na za sasa yanayowafanya vijana kuishia jela kwa makosa ya wizi , ubakaji na mengine .Si kwambii ni mambo gani wewe mwenyewe umeshayajua. Mambo tuliyoyaundia tume na vikosi kadhaa vya kupambana nayo ...lakini wapemba wasema , nkuchukua maji kwenye fuu tomo ama maji kwenye pakacha .
Nimeanza kwa kicha cha habari "Jumba la Dhahabu".Najua hapa fikra zako zitaanza kukupeleka kwa Jini Kabula ,Kojac , Mzee Chilo na wengine ;wasanii waliobobea katika fani ya maigizo ya luninga . Mi siko huko akhui, usiwe na haraka za chura ,,,ukaruka ukangia mumo!
Kwa mitaa ya Machomane ukizungumza upelekwe Jumba la Dhahabu , hee watu watakushangaa .Kama una joho na kilemba watakwamia , ssalaleee mjomba hata weye ? Lakini Wapemba wana msemo wao maarufu , "Nkongwe haina shehe!"
Ndio hivyo majumba ya dhahabu yapo yamejaaa .Si Machomane tu mtaa nilioufananisha na Miembeni ya Unguja lakini hata Msingini , Kichungwani , Wawi majumba hayo yapo .Wapemba wasema n’dezo biashara ni mapatano.
Ndio wamehamia na majumba wamekodishwa na wazawa ambao wanasifika kwa kuswali na manundu ya sijida .Wengine wanasema ni watu kutoka ‘waja leo , warudi leo kule kunakotajwa ndio makao makuu ya mahaba dunia ;Simba anakongolewa sharubu na akapigishwa msuaki.Wenyewe ukiwauliza wanasema wamekuja kutafuta maisha kwani Zanzibar biashara ipo wanunuzi wa kumwaga . Wanajitahidi kutangaza mitaani , kwani waswahili wanasema biashara itangazwayo ndio itokayo .Hawana mazoea ama kutunza utamaduni wa Kizanzibar wa kufaa matandio , maninja na mashungi , wala .Wanavaa za kisasa na wapitapo mitaani huambiwa , Muungano udumuuu! Na ni kweli muungano unadumishwa na faida ya muungano inaonekana .
Biashara inaenda kwani wenyewe wanasifu kwamba kutokana na vigenzo vya kumlinda mlaji bidhaa inauzika .Na kwa nini wasiuze walaji wapo .Kwani unadhani wanakula watu wa mbali ; ndio hao hao bin kinaanata bin huzaimata bin ilyasa.Wenye wake zao waliotulia majumbani .Au vijana wadogo wa shule ambao ndio kwanza hawajajua utamu wa pilau , wameujulia kwao!
Sisemi maneno haya kwamba labda miongoni mwa wauzaji na wenye mji hawamo .La hasha wapo tele . Wengine ndio hao hao baadhi yao wanaovaaa tarabizuna na ninja ili wanapokatisha mitaani wasionekane . Na wala sithubutu kusema kwamba kila waliotoka huko na kuja kupanga kwamba wanafanya hivyo , la hasha .Wapo waungwana na heshima zao .Wamekuja kutafuta maisha.Wanajituma na kutafuta riziki kwa bidii. Wameanzisaha biashara zao na maisha yanakwenda .Wamewaacha wenyeji wakikaa barazani na kuzungumza mambo ya harusi.Kupigana michango ya kila siku ya machai ya harusi na maholi ya rusha roho.Kwao si shida kukipata kila kitambaa au fasheni ya baibui inayoingia mtaani . Wana wasiwasi gani na allah riziki analeta
Nakumbuka siku moja nilikua na kajiutafiti kidogo pamoja na wenzangu .Miongoni mwa tuliozungumza nao ndio hao hao kamata mkia chinja . Mmoja alipoulizwa kwa wiki unaweza kuuza bidhaa kwa watu wangapi alisema , “ Naweza kupata watu 10 , saba hadi sita’’. Kwa bei ya shilingi ngapi akasema .Ndio hivyo hivyo tu, wengine wanakula baadae hawalipi , lakini sh elfu saba nane hadi tano” . Alipoulizwa tena kama umekosa mteja huna pesa unafanya nini”” Basi alijibu unajua wengine ni maarufu hapa .Tunabadilisha bidhaa kwa bidhaa ….kama kilo tatu za mchele , lakini ukikosa unakwenda hata kwa 2000.Unadhani tutafanyaje na maisha magumu” Alisema
Haya kama bidhaa imefikia kuuzwa kwa shilingi 2000 unadhani nani atashindwa kununua .Unajua wazee wengine pesa kama hiyo anampa kijana wake atumie shule kila siku .Ndio yaliyomkuta kijana mmoja ambae sitomtaja jina .Alikua akipewa pesa za kutumia skuli anakusanya na zinapotimia elfu 4000 tu anakimbilia majumba ya dhahabu .Hakujuilikana na na wazazi wake hadi alipopata maradhi ya kuambikiza (kaswende) .Siri ikatoboka kwani alipobanwa na wazazi wake alitoa ushuhua pamoja na kuwataja marafiki zake wote wenye mchezo kama huo .
Naandika nukuu hii nikiwa na wasiwasi sana kwamba huko twendako na vizazi vyetu siko .Sikatai kufaidi matunda ya muungano wala siipingi kauli ya kwamba Zanzibar ni njema na atakae aje, bali nakihofia hichi kizazi na haya maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI
.Zanzibar ni ndogo sana.Mitaaa ina watu kidogo sana .Kama itakuepo tabia ya kubadilishana bidhaa basi sijui khatima yake nini
Pale mwanzo tulikariri kauli mbiu ya mapambano dhidi ya UKIMIWI yaani A-Acha kabisa, B-Be Faithfull yaani kuwa muaminifu na mkeo, nay a tatu C - Use Condom .
Du hii C inaleta mijadala kila unapoitaja .Lakini kinachoonekana kwa sasa A inaanza kushindwa nguvu , B ni ya wachache waliookoka , na C haipatikani hata inapohitaji na maadili hayaruhusu kutumia . Hapo ndipo penye kitendawili cha Tembo kutengwa kwa ubambe kwani wenye bidhaa wanasema , chakula ni cha hoteli mlaji ana hiari yake .Kula kwa kijiko ama mkono mtupu . Lakini kwa kauli yao mmoja alisema wengi wa wateja hawapendi kula kwa kijiko, eti wanakosa ladha.Wanalazimisha mkono mtupu na wanapofanya hivyo bei ya chakula huongezewa na huridhia kama kuku anaetaga .
Nakumbuka zamani nilipokuwa nafunzwa masuala ya kuchochea mabadiliko ya tabia niliambiwa kwamba kuna mikabala mengi ya kufanywa na jamii kama jamii imedhamiria kuondosha maovu .Mkabala mmoja nitakuhadithia .Kama ni mkaazi wa Unguja bila shaka umeusikia ujasiri wa watu wa miembeni waliposema vilabu vya pombe chini ya mapaa ya nyumba zao basi.Walinyanyua sauti.Wakatishia kuchukua hatua mikononi mwao iwapo serikali itashindwa .Waliamua hivyo kwa sababu waliona kuwepo kwa vilabu hivyo ni tatizo kwao na familia zao.Pombe ziliuzwa kama maji ya kunywa .Wanouza miili yao wakaona ndio sehemu pia ya kujipatia wateja .Baraza za majumba yao zikawa ndio magodoro ya kufanyia ngono giza liingiapo.Magamba ya kondom yakazagaa kila chochoro ya mtaa .Majumba ya dhahabu yakawepo kila kona na watoto wakajifundisha kula bata bila manyoya .
Basi wakaazi hao wakaona uchungu.Serikali baadae ikachukua hatua kwa kuziondoa baa hizo.Hivi karibuni nimesikia kuna mikakati ya kuyaondoa majumba ya dhahabu .Toba sikio , nasikia hivi karibuni nyumba moja iliungua moto sambamba na baa maarufu Jonzani .Haya wa Miembeni lakini kama hili linawachoma mbona madawa ya kulevya yanauzwa mchana na mumetulia .Vijana wanaangamia ?
Nisiseme sana kama nimemeza vocha ya dola 50.Nilichokusudia kusema Pemba ni ndogo sana .Mzunguko wa watu ni wa wale wale.Iwapo maambukizi ya UKIMWI yatakuwepo kwa makundi Fulani ya watu basi watu hao hao huwa na muungano mkubwa na jamii yote kiasi ambacho ni mwanya kwa virusi kusambaa hata kwa yule alietulia nyumbani akimsubiri bwana alete mapembe .
Bado kazi ipo ya kupambana na matatizo haya nikiitupia jukumu jamii yenyewe kuwa chanzo cha mabadiliko.Majumba ya dhahabu yapo na yanaendelea kuwepo lakini bado tunaweza kutumia mikabala ya jamii kwa njia za ustaarabu na kubadilisha hali hii .