Powered By Blogger

Tuesday 23 February 2010

JASIRI HATUNAE TENA

NA   ALLY   MBAROUK OMAR
BWANA SALUM ALI SALUM


ZANZIBAR YAPOTEZA SILAHA YA MAPAMBANO YA UKIMWI


SHUHUDA JASIRI ,JEMEDARI HATUNAE TENA

Marehemu  Bwana Salum  Ali  Salum   akifungua moja kati ya  vikao  vya kupambana na UKIMWI


Ya rabi mola mananiiiii ……..oooooooooh
Utupe Kinga na tiba
Ugonjwa huu jamaniiii……..aaaaah
Usiwe kwetu msiba
Vijana wavitandaniiiii ……….aaaaah
Wao pamoja na baba…ooooh
Sote tuko mashakani ……….eeeeeeh
Ukimwi jama ukimwi ……..iiiiiih
Mola tupe , kinga na tiba .

    Pengine umeshawahi kuusikia wimbo huu ; ukiimbwa kwa sauti nzuri inayoweza kumtoa nyoka pangoni. Basi kama hujausikia pengine uliwahi kuhudhuria katika maadhimisho ya kitaifa ya siku ya Ukimwi duniani mwaka 2008 hapo katika uwanja wa Gombani ambapo mgeni rasmi alikua ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Amani Karume .



Basi sauti hii ni ya jasiri, shuhuda aliyejitolea katika mapambano dhidi ya Ukimwi marehemu Salum Ali Salum au maarufu , Bwana Salum au sisi tuliomzoea tulikua tunamwita tu Samandalo yaani Babu lao .
Alikua mcheshi mpole aliejaaa hekima na busara .Alimheshimu kila mtu mdogo kwa mkubwa .Unapokaa na bwana Salum utakata mbavu tu, maneno yake ni matamu kama asali au unaweza kumwita ‘kidomo sukari’.Alipokua hospitali Muhimbili kabla ya kuenda Tanga ambako mauti yalimchukua nakumbuka tulikua tunazungumza mara kwa mara .Daima sauti yake ni ya busara na mtulivu sana .Nakumbuka siku moja baada ya kumjulia hali aliniuliza . “Mapambano yanaendeleaje huko?”.Daima alitoa ushauri nini tufanye pale penye matatizo na changamoto”
Kama kujishughulisha na mapambano dhidi ya Ukimwi unatunukiwa nishani za jeshi na mimi nikawa ndio amiri jeshi mkuu basi bwana Salum Ali ningempa nishani ya juu ya utumishi wa jeshi yaani Field Masher ikiwa hichi ndio cheo cha juu. Nasema hivi kwa sababu alikua mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya Ukimwi hapa kisiwani Pemba au Zanzibar kwa jumla .
Nakumbuka enzi zile hapa kisiwani Pemba ambapo anaeishi na virusi vinavyosababisha UKIMWI alionekana ni kama balaa; watu wakasutwa , wakasemwa kwa maneno mabaya na kutengwa katika jamii .Basi yeye kwa ujasiri wake akawa mtu wa mwanzo kujitokeza hadharani kwa Pemba na kuzungumzia hali yake .Hakuona aibu ya kuzungumza na vyombo vya habari kwa uwazi na ufasaha .Akawaelimisha wengine na kuwapa faraja .Akawa kimbilio la ushauri kwa watu waliopatwa na tatizo kama lake .Alijitolea muda wote katika mapambano na kamwe hakua mbabaishaji wala mwenye tamaa .
Nakumbuka siku moja tukiwa katika uhamasishaji huko Kangani pale aliposema “ Watu hawaniamini nikisema kwamba naishi na virusi.Wanasema nimepewa pesa na Serikali ili nielimishe Ukimwi.Wanasema bwana Salum wewe muongooo , mtu mwenye Ukimwi atakaa hivyo? Basi niwaambie Ukimwi upo na hapa Kangani upo na mimi naishi na virusi.Kama hamuamini kadi yangu ya dawa hii” Maskini akaitoa kadi yake ya kuchukulia dawa za ARV hadharani , watu wakamshangilia kwa ujasiri wake .
Ndivyo alivyokua Bwana Salum ambae alikua na ari na nia ya kweli ya kuwaelimisha wengine.Ujasiri na uimara wake ulikua mkubwa mno kwani kwa kujitolea alianza kuwatafuta na kuwashauri watu wenye hali kama yake ili wawe na sauti moja na vilio vyao visikike ;visiwe vilio vya samaki machozi kwenye maji .
Dk Juma Massoud wa WAMATA Pemba alisema . “ Kwa kweli ilikua ni kazi ngumu ya kuwakusanya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi pamoja ,lakini yeye alitusaidia na bila msaada wake tungalikwama”.Alisema na kutanabahisha kwamba WAMATA wametoa mchango mkubwa kusaidia
Waswahili wanasema papo kwa papo kamba hukata jiwe na umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.Ndio kazi aliyofanya bwana Salum ya kuwaunganishwa watu pamoja hadi hapo ilipozaliwa rasmi Jumuia ya Watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi Pemba ,ZAPHA+.Hii ilikua ni kwa ajili ya kuunga nguvu jumuia hiyo ambayo makao makuu yapo Unguja . Na mara tu ilipoundwa na wanachama kukaa pamoja juhudi zilifanywa za kutafuta uongozi .Ninakumbuka siku ya uchaguzi uliofanyika Ukumbi wa TC chachani .Unadhani kulikua na mgombea mwenza .Unadhani alipiga kampeni ….wala ! Wanachama walimchagua kwa ushindi wa kishindo kama si wa sunami! Alishajitangaza .Hakua na mpizani .Unadhani nani angejitokeza , labda angepata hiyo kura yake tu!
Hayo alifanya kwa nia ya dhati hadi hivi leo wanajumuia wanatambulika kwa kazi yao nzuri wanayofanya .Wamesaidaia sana harakati za mapambano hasa katika kupunguza unyanyapaa .Hivi leo nani asietambua mchango wa ZAPHA+ ambapo kwa ujasiri wao wamejitokeza na kufungua matawi kila wilaya hapa kisiwani Pemba kiasi cha kufikia wanachama 235 kwa sasa .Hii ni hatua kubwa kwani hapo awali aliejitokeza alikua ni jemedari huyu tunaemzungumzia .
Leo ZAPHA+ kwa juhudi zake na wengine imesimama.Wanachama wamejikusanya pamoja na kufanya mambo mengi ya kutoa elimu na miradi midodo midogo ya maendeleo
Ndivyo alivyokua .Alikua mtu wa watu ,anaependwa na kila mtu .Labda nisimwagie sifa peke yangu.Nilipozungumza na mwenyekiti wa Zapha+ , Consolata John mara baada ya msiba huu , mwanzo alisema .



“Hili ni pengo kubwa si kwa Zapha+ Pemba tu bali kwa Zanzibar nzima” Ndivyo alivyomuelezea marehemu bwana Salum na kuongeza , “Alikua mchapa kazi asiechoka .Alietumia muda wake mwingi kujitolea kwa hali na mali kwa kazi za jumuia .Alikua ni kiungo muhimu .Kweli tumeondokewa na mchapa kazi hodari” Alisema Consolata kwa huzuni
Nikizungumza na mmoja wa wataalamu anaefanya kazi kwa karibu na ZAPHA+ , Seif Juma alizungmza mengi yanayomuhusu Bwana Salum.Alisema si kwamba hakua mtu alieshika nafasi za uongozi hapa Zanzibar tu bali hata ndani ya Afrika ya Mashariki . “Alikua ni mjumbe wa Bodi ya Mtandao wa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi wa Afrika Mashariki pia akiwa kama ni mweka hazina wa jumuia hiyo .Hii kwetu ni heshima kubwa kwa mzanzibari kushika wadhifa kama huo” Alisema Seif na kuongeza kwamba ,Bwana Salum alikua mtu muelewa wa mambo mengi na aliisaidia sana jumuia .



Nae mratibu wa Tume ya Ukimwi Pemba , Nassor Ali Abdalla alimtaja Bwana Salum kama kiungo muhimu sana cha mafanikio, . ‘’Hapa tumepoteza mtu , alikua ni kiungo muhimu kati ya Tume ya Ukimwi ,ZAPHA+ na jumuia nyengine”.
Pengine bwana Salum aliona kwamba pamoja na kuwepo ZAPHA+ bado juhudi zilihitajika za kuanzisha jumuia nyengine za maendeleo na mapambano ya UKIMWI .Mnamo mwaka 2007 alikua mwanachama muanzilishi wa jumuia ya JUKUVUM ( Jumuia ya Kupambana na Virusi vya Ukimwi Mkoani ) .Jumuai hii kwa sasa inaendelea na miradi mingi ya mapambano ya UKIMWI.Pamoja na nafasi hii pia alikua ni mjumbe wa Kamati ya Wilaya ya UKIMWI nafasi ambayo ameitumikia kwa mafanikio makubwa .
Mara tu baada ya kutokea msiba wa kifo chake ,mtaa wa Mkoani Mapinduzi ulikua kimya .Anasimulia Moh’d Rashid mkaazi wa hapo .


“Kama siamini hivi, naona kama tutapishana njiani sasa hivi.Yaani siamini” Alisimulia .


Hivyo ndivyo alivyokua .Nyumba yake alipokua anaishi ilipachikwa kila majina .Wengine waliita Angaza.Hii ni kwa sababu pia alitumia kama sehemu ya kuwapa watu ushauri nasaha kwa anaepata tatizo kama hilo .Alihudumia wagonjwa , kuwapa faraja na misaada ya hali na mali .Aliwafata popote walipo tena kwa kutumia nauli yake si ya jumuia pale lilipotokea tatizo . Kazi hii aliifanya kwa nia safi, bila malipo wala ushuru wowote akishirikiana na mke wake mpendwa , Bi Aisha Rashid


Familia yake yote kwa hapa Pemba ameihamasisha vizuri .Watoto wake akina Fatma na Zahra ni waelimishaji wazuri katika jamii.Kwa kupitia klabu ya watoto au ToTO KLABU wameanzisha kikundi cha uhamasishaji na siku zote huwamwaga watu machozi katika mahafali mbalimbali za kuelimisha jamii kwa kutoa ujumbe wenye hisia kali .


Mke wake mpenzi Bi Aisha Rashid pamoja na kazi kubwa anayofanya ya uhamasishaji pia ni mshauri nasaha katika kituo cha MCT na CTC Mkoani na anafanya kazi hiyo kwa mafanikio makubwa .Yeye mwenyewe anajulikana kwa jina la “MAMA USHAURI”
Kama kuma kuna mtu anahitaji kupewa sifa kubwa kwa kupambana na vitendo vya kuwadhalilisha na kuwatenga watu wanaoishi na virusi vinavyosababisha UKIMWI kwa Pemba basi Bwana Salum ni namba moja . Ni yeye alietilia mkazo kuanzishwa kwa kampeni hii na kuwashawishi wengine wajitoe kupambana na unyanyapaa. Basi wana ZAPHA+ wakaungana na kampeni hii kwa nia ya dhati hasa kwa kutoa ushuhuda . Kwenye mikutano ya hadhara, semina na warsha , kwenye majimbo na shehia kote wakafika huko kuelimisha wananchi . Jasiri huyu akawa mstari wa mbele kuhamasisha hadi hii leo mipapai iliyochumwa na mtu mwenye VVU haikatwi tena na maandazi barabarani yananunuliwa . Leo hii ninapoandika makala hii ZAPHA+ si tatizo katika jamii bali ni suluhisho la kukimbiliwa na wengi.
Kwa ujasiri huu na kushirikiana na taasisi kama vile ZAC , WAMATA , USAID , CLINTON FOUNDATION ,ZACP , CVM wana Zapha wakajitoa . Sasa wanatumika kutoa ushauri nasaha katika hospitali kubwa, kutoa na kusaidia huduma majumbani pamoja na kujikusanya pamoja na kuanzisha miradi ya maendeleo . Kama si juhudi za kamanda huyu aliekua na kipaji kikubwa cha kuunganisha watu , yote haya yasingefikiwa .
Maisha ya familia ya bwana Salum ni ya furaha yaliyojaaa matumaini. Wote ni wana mapambano dhidi ya Ukimwi.Muambata wake mkuu ambae ni mke wake kipenzi , hadi Bwana Salum anaaga dunia , nae ni jasiri mwenye uthubutu katika mapambano.Wote kwa pamoja walijitoa hadharani na kuelimisha jamii .Si jambo la kushangaza kupanda jukwaani pamoja na kuelimisha kuhusu Ukimwi.Siku moja tukiwa katika kampeni ya kupambana na unyanyapaa kwa Wilaya ya Mkoani nakumbuka walisimama pamoja na kuimba wimbo huu.
Twende wapi twende wapie eee mama eee mama
Tumueleze nani matatizo yote sisi wana Zapha @2
Mitaani wanatukataa
Majumbani wanatunyapaaa
Ee mola tusaidie
Tuna kilio eeeh
Tuna kilio eeeeeh …..mama
Twende wapi , twende wapi ooooooh mama @2
Tumueleza nani matatizo yetu yeeetu , sisi yatima
Tumueleze nani matatizo yetu , sisi kama yatima
Wakiimba wimbo huu kwa hisia kali na vibwagizo , watu walibubujikwa na machozi .Nakumbuka alikuwepo Naibu Katibu mkuu , Mhe Msham Abdalla Khamis ambae ni rafiki mkubwa wa Bwana Salum. Katika hotuba yake aliyoitoa mkutanoni hapo , Mhe Msham hakuacha kumwagia sifa jemedari huyu wa mapambono kwa kumtaja kwamba ni mtu wa aina yake mwenye kila sababa ya kupongweza kwa jukumu zake za kuelimisha jamii. Nikuhadithie kitu , kwa ushawishi wa Bwana Salum na ari ya Mhe .Msham ya kuungana na jumuia hiyo alichukua uanachama wa jumuia ya ZAPHA+ akiwa ni mtu kama wa pili aliejiunga na jumuia hiyo pasi na kuwa anaishi na virusi.Katiba ya jumuia ya ya ZAPHA+ inaruhusu kwa watu wengine kujiunga na jumuia hata kama huishi na virusi vinavyosababisha UKIMWI .
Kwa wakaazi wa mjini Tanga handeni takriban miaka kama 35 iliyopita jina la Salum Ali Salum lilikua maarufu sana.Alisifika kwa sauti yake nyororo na manjonjo apandapo jukwaani akiwa na kikundi cha taarab .Nakumbuka siku moja enzi za uhai wake alinihadithia

“Aaaa bwana Ali , enzi hizo Salum nikiwa Salum nilikua natisha kwenye taarab” Alisema hapo akaniimbia kipande cha mashairi ambacho leo sikikumbuki tena na baadae akacheka sana na akaniuliza . “Niambie , hapo vipi”. Sikuwa na jipya ni zaidi ya kumkubali tu na kugonga kiganjani kwake . Unajua bwana Salum alikua anapenda kujichanganya na alikubalika na watu wa umri wote .Akikaa na wazee atakua kama wao , lakini akikaa na vijana kama sisi , aaah tulipiga stori hadi basi huku tukikata mbavu kwa utani na mizaha yake .
Ni nani angalikubali kama utamkuta Bwana Salum na kaunda suti zake , kiatu kikali mguuni na bashasa zake na akakueleza kwamba ana miaka 68 akizaliwa mwaka 1942 !Kamwe utabishana nae tu .Alikua anajipenda sana na siku zote alikua smart ,msafi na mtanashati.

Pamoja na wasifu wake mkubwa wa kuitumikia jamii , pia Bwana Salum alikua mtaalamu .Aliwahi kufanya kazi pia na General tyre huko Arusha kama muhandisi
Mwaka 1999 alihamia kisiwani Pemba na alipofika tu aliendelea na kazi yake ya ufundi mifereji kama kibarua chake binafsi .Alikua fundi muadilifu na umahiri wake wa kufanya kazi hii ulimuongezea sifa na kuwafanyia watu wengi kazi hiyo . Kwa maeneo ya mkoani alijulikana pia kama fundi Salum
Jina la Samandalo kwa nyumbani kwao kijiji cha Nandiamba Wilayani Handeni-Tanga lina maana ya “babu yao” ,lakini mwenyewe enzi ya uhai wake alilikuza na kuliita “babu lao”.Ndio hivyo kwani hadi anafariki dunia usiku wa tarehe 15/ 2/2010 kijijini kwao Tanga , akiwa na umri wa miaka 68,aliacha watoto 17 , mjane mmoja na wajukuu 25 .Bila shaka jina la Samandalo au babu lao liliendana na barka yake ya kizazi na wajukuu wengi aliobarikiwa .Nilipomuuliza mke wake ,Bi Asha Rashid unadhani bwana Salum kaacha vitukuu vingapi nakumbuka aliniambia , “Ah! Hilo ni suala gumu kwani inabidi niwapigie wajukuu zake wote walionza kuzaa na wengine namba zao za simu sina!” Alisema na nilimwambia basi kwani haya uliyonieleza yanatosha
  Marehemu Bwana  Salum  Ali   Salum (katikakati)  akifungua  kikao cha TAC  Pemba


Waswahili wanasema pang’okapo jino hukaa pengo na ni kweli .Kwa kuondokewa na shuhuda jasiri huyu pengo gego aliloliacha kamwe haliwezi kuzibika . Ni taa iliyozimika ambayo muangaza wake uliwafikia wengi .Alileta matumaini pale wenzake walipokata tamaa.Akawatia moyo na ujasiri wa kuwaokoa wengine .Hakuwa na kiburi na dharau .Alichapa kazi bila kuchoka kama analipwa madola ya shilingi.
Nakumbuka mengi aliyoyaanzisha .ZAPHA+ Pemba imezaliwa na inatambaa .Badi inahitaji mbeleko za jasiri huyu.Walezi wengine wapo na wanajituma lakini hii ilikua nguzo iliyosimama vyema.


Tumalizie kwa tauhidi ;aandikali mola halifutiki na kalamu ya mola haina makosa .Mungu amlaze mahala pema peponi .AAAMIN RABI AAMINA

No comments:

Post a Comment